Pages

Thursday, 21 April 2016

Rafu yamwondoa Kessy Simba

  • Safari ya Azam, Yanga yanukia
  • Tippo adai watafanya biashara na timu yoyote


RAFU mbaya aliyoicheza beki mahiri wa Simba, Hassan Kessy dhidi ya mchezaji wa Toto African, Edward Christopher, imemsababishia kutemwa kuitumikia timu yake hiyo hadi mwisho wa msimu huu.

Kessy alimchezea rafu Christopher kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha kutolewa nje kwa kadi nyekundu, huku uongozi wa Simba ukimuongezea adhabu ya kukosa michezo yote iliyobaki katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbali na kusimamishwa kwa mchezaji huyo, tayari kuna tetesi za kuikacha klabu hiyo na kujiunga na kati ya klabu ya matajiri wa Bongo, Azam au Watoto wa Jangwani, Yanga, licha ya tetesi hizo kutokuwekwa wazi.

Inadaiwa timu hizo Azam na Yanga zilikuwa zinasubiri kumalizika kwa michezo yao ya kimataifa ya marudiano kati ya timu za Esperance na Kombe la Shirikisho na Al Ahly mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ili zianze mchakato wa kumnasa beki huyo ambaye mkataba wake unaisha mwezi Juni.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kessy alisema bado uongozi haujampa taarifa zozote za kusimamishwa kwake.

“Sijapewa taarifa yoyote, lakini kama wameamua kunipa adhabu sawa nitaitumikia kwa kuwa bado ni mchezaji wao na bado nina mkataba nao, ila nikimaliza mkataba wangu mwezi wa sita meneja wangu ataamua kama nitabaki au nitaondoka,” alisema.

Kwa upande wa meneja wake Athuman Tippo, alisema wamepokea maamuzi ya uongozi huo kumsimamisha mchezaji wake na ataitumikia adhabu hiyo kama ilivyoamuliwa kwa kuwa ni mwajiriwa wao.

“Ataitumikia adhabu yake hadi atakapomaliza mkataba, lakini bado tunaendelea kusubiri adhabu watakayompa Vicent Angban na wasipofanya hivyo tutaendelea na msimamo wetu wa kuchukua hatua zaidi, tutakaa na mwanasheria na kupanga nini tufanye baada ya kipa huyo kujichukulia sheria mkononi kumpiga Kessy,” alisema.

Alisema hadi sasa bado hawajafanya mazungumzo na timu yoyote nyingine, lakini Kessy akimaliza mkataba wake atakuwa huru hivyo watafanya biashara na timu yoyote itakayomtaka.

Kessy jana alitangazwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, kuwa atakosa michezo yote iliyobaki katika ligi, akieleza alionekana kucheza rafu mbaya ambayo ingeweza kumsababishia kifo mchezaji huyo wa Toto.

“Kessy ameihujumu timu kwenye mchezo huo kwa rafu mbaya aliyoicheza, iliyosababisha kupewa kadi nyekundu kwani hakuwa na sababu ya kucheza vile alionekana kabisa ameinua mguu sijui ni makusudi au bahati mbaya, angeweza kumsababishia hata kifo Edward, hivyo tumeamua kumuongezea adhabu badala ya kukosa mechi mbili kwa kadi aliyopewa atazikosa mechi zote tano,” alisema.

Hata hivyo, mchezaji huyo mbali ya kucheza rafu hiyo iliyomuondoa Simba, alikuwa anaandamwa na jinamizi la kutoaminika tena Simba tangu alipoigharimu klabu yake katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kati ya Simba na Yanga iliyochezwa Februari 20 kwa kuokoa mpira kizembe ambao ulinaswa na mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma na kufunga bao kirahisi.

Na Mwali Ibrahimu/ Mtanzania
Video : Mafoto

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here