Mshambuliaji wa Simba, Brian Majwega akikwepa mguu wa mchezaji wa Singida United, Ponzi Mgeni wakati wa mechi yao ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.
SIMBA jana ilimaliza hasira za kufungwa na Yanga kwa Singida United baada ya kuichapa mabao 5-1 na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA.
Mechi hiyo ni ya kwanza kwa Simba tangu itoke kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa mtani wake Yanga katika mechi ya Ligi Kuu bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Februari 20 mwaka huu.
Simba ilitawala asilimia kubwa ya mchezo wa jana tangu mwanzo wa kipindi cha kwanza na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Dan Lyanga aliiandikia Simba bao la kuongoza katika dakika ya tatu kabla Hamisi Kiiza hajaongeza la pili katika dakika ya 21.
Kiiza alifunga bao hilo baada ya kipa wa Singida United, Jacton Munna kuanguka ambapo aliuwahi mpira na kuujaza wavuni.
Kiiza aliifungia Simba bao la tatu katika dakika ya 66 kwa kichwa baada ya kuunganisha pasi ya Brian Majwega. Bao la nne la Simba liliwekwa kimiani na Awadhi Juma katika dakika ya 83 na dakika tatu baadae alifunga bao la tano.
United ilipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 90 likifungwa na Paul Malamla. Aidha Simba ingeweza kupata mabao mengi jana kama washambuliaji wake wangezidisha umakini kwani walikosa mabao ya wazi mfululizo.
Kiiza alikosa bao dakika ya 13 na Lyanga alikosa dakika ya 16 baada ya wote kupiga mipira nje wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga.
Kutoka kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza mwandishi Alexandra Sanga anaripoti wenyeji Toto Africans walishindwa kutumia vema uwanja wao baada ya kuchachapwa bao 1-0 na Geita Gold.
Bao la Geita lilifungwa na Chibuga Chibuga katika dakika ya 64 baada ya kupata pasi ya Juma Nade.
GRACE MKOJERA / HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment
Want to comment? write down here