Pages

Wednesday, 17 February 2016

Jonesia kuamua Simba na Yanga


MWAMUZI Jonesia Rukiyaa wa mkoani Kagera, amepewa jukumu la kuchezesha mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga, katika mchezo wao unaotarajiwa kuchezwa  Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamuzi huyo mwenye beji ya Fifa, anaingia uwanjani kuzichezesha timu hizo kwa mara ya pili baada ya kuzihukumu katika mechi ya Nani Mtani Jembe 2014 ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 2-0.

Katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki, Jonesia atasaidiana na Josephat Mburali (Tanga) na Samwel Mpenzu (Arusha), huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Eli Kasihili wa Dar es Salaam,  wakati kamishna wa mchezo huo akiwa Khalid Mutego kutoka Mwanza.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka nchini (TFF), jana lilitangaza viingilio katika mchezo huo huku kiingilio cha chini kikiwa ni Sh 7,000.

Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, alisema kwa viti vya machungwa kiingilio kitakuwa  Sh 10,000 , VIP C na B ikiwa  ni Sh 20,000  huku VIP A ikiwa Sh 30,000.

Alisema tiketi zitaanza kuuzwa Ijumaa  katika vituo mbalimbali ikiwemo kwenye Ofisi za TFF Karume, Kidongo Chekundu, Uwanja wa Taifa, Dar Live, Buguruni sheli, Ubungo Oil Com, Steers, Feli na kituo cha mabasi Makumbusho.

Kizuguto aliwataka wadau pamoja na wapenzi wa mpira kununua tiketi hizo katika sehemu husika, ili kuepukana na matatizo ya kununua tiketi ambazo sio halali.

“Tunawaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo, ili kila mmoja aweze kuburudika na kushangilia timu yake ambapo ulinzi utakuwepo na umeimarika kwa kushirikiana na vyombo vya usalama,” alisema.

THERESIA GASPER, NA SUZANA MAKORONGO (RCT)
MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here