Pages

Sunday, 17 January 2016

Mayanja aanza vizuri na Simba


Kocha Jackson Mayanja ameanza vyema kibarua chake Simba, baada ya kuiongoza timu hiyo kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Hamis Kiiza aliifungia Simba bao hilo pekee katika dakika ya tano akiunganisha kwa kichwa krosi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na kumfanya Mayanja kutembea kifua mbele.

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 30 na kuziongezea presha Azam na Yanga zilizazoongoza ligi hiyo kwa sasa, huku wakishusha Mtibwa hadi nafasi nne.

Katika mchezo huo, Mtibwa ilionekana kuzidiwa na kushindwa kuhimili kasi ya mashambulizi ya washambuliaji wa Simba, lakini umakini mdogo wa Kiiza, Ajibu uliwanyima wenyeji hao nafasi ya kupata mabao mengi.

Kipindi cha pili, Mtibwa ilirudi kwa kasi na kufanya shambulizi kali dakika ya 52 baada ya Ibrahim Jeba kuambaa na mpira na kuachia shuti lililogonga mwamba na kurudi uwanjani na mabeki wa Simba kuokoa.

Kiungo Justice Majabvi wa Simba alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 13, kwa kumchezea rafu Shiiza Kichuya, pia dakika ya 22 Henry Joseph wa Mtibwa alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Peter Mwalyanzi.

Katika michezo mingine iliyochezwa jana, kocha Abdallah Kibadeni alishuhudia timu yake ya JKT Ruvu ikipokea kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Mgambo JKT.

Stand United ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, shukrani kwa goli lililofungwa na Revocatus Richard katika dakika ya 12.<

Coastal Union ililazimishwa sare 1-1 na Majimaji jijini Tanga. Coastal Union ilipata bao kupitia Absalim Chidiebele kabla ya Alex Kondo kuisawazishia Majimaji.

Jijini Mbeya wenyeji Mbeya City ilichapa Mwadui bao 1-0 lililofungwa na Ditram Nchimbi katika dakika ya 49, lakini         City ilipata pigo baada ya kiungo wake Haruna Moshi ‘Boban kuonyeshwa kadi nyekundu. Mshambuliaji Jeremia Juma aliingoza Prisons kuichapa Toto African bao 1-0 jijini Mwanza.

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here