KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja, amesema anaandaa mbinu mpya ili aweze kuifunga Yanga katika mchezo wao wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mayanja ambaye ana rekodi nzuri katika kikosi hicho tangu alipoanza kukifundisha Januari mwaka huu baada ya Dylan Kerr kutimuliwa, amepanga kutumia mbinu mbadala ili waweze kuifunga Yanga na kulipiza kisasi.
Timu hizo zilipokutana katika mzunguko wa kwanza, Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, waliibuka kidedea kwa kuwanyuka watani wao hao mabao 2-0.
Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa, Mayanja alisema ameandaa programu kwa ajili ya Yanga kwani anahitaji ushindi ili waweze kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Alisema anaamini mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na mahasimu wao kupata uzoefu katika michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya juzi kuwafunga wapinzani wao Cercle de Joachim bao 1-0 walipocheza ugenini nchini Mauritius.
Kocha huyo raia wa Uganda, alisema mchezo huo umewasaidia Yanga kujiandaa dhidi yao na atahakikisha atatumia mbinu tofauti kuwakabili watani wao wa jadi baada ya kupata pointi sita katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
“Tutatumia mbinu tofauti kabisa ili kuhakikisha ushindi unapatikana, Yanga wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika michuano ambayo imekuwa ni sehemu ya kujiandaa na mchezo dhidi yetu,” alisema Mayanja.
Simba inatarajia kuweka kambi mjini Morogoro kujiandaa na mchezo huo, ikiwa ni baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Matokeo hayo yameifanya Simba ifanikiwe kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufikisha pointi 45 na kuishusha Yanga iliyopo nafasi ya pili ikiwa na pointi 43 huku Azam FC yenye pointi 42 ikishika nafasi ya tatu.
Mtanzania
0 comments:
Post a Comment
Want to comment? write down here