Dar es Salaam. Ngonjera kuhusu ujenzi wa uwanja wa kisasa wa klabu ya Simba zimehamia mwaka 2016, huku ikielezwa kuwa tayari klabu hiyo imepata mwekezaji. Uwanja huo ulioko Bunju, nje kidogo ya Dar es Salaam umegeuka hekaya za viongozi wa klabu hiyo kwa muda mrefu sasa.
Jana, kiongozi mwandamizi wa klabu hiyo aliliambia gazeti hili kuwa wapo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba na mwekezaji huyo mzawa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja wao na ujenzi kupangwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi.
Klabu hiyo, pia ilithibitisha kupata mwekezaji aliyetajwa kuwa ni Mtanzania na kwamba hadi kukamilika kwa uwanja huo utagharimu zaidi ya Sh2 bilioni.
Rais wa klabu hiyo, Evance Aveva hakuwa tayari kukubali wala kukanusha kufikiwa kwa hatua hiyo.
Awali, kiongozi huyo wa Simba alilithibitishia gazeti hili kuwa makubaliano baina ya pande hizo mbili yamefikia hatua nzuri.
Kiongozi huyo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo alisema mchakato wa kupata mwekezaji na ujenzi umefikia hatua ya makubaliano ambayo yako katika hatua za mwisho na wakati wowote mwezi huu ujenzi utaanza.
“Tayari, tumepata mwekezaji mzawa amekubali kujenga uwanja wetu na kwa kweli tuko katika hatua nzuri na niwaambie wapenzi na mashabiki wetu (Simba) hadi kufikia Januari 30, wataanza kuona mabadiliko kule Bunju,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Hadi kukamilika ramani yetu ya mwanzo ilionyesha tutatumia sh2bilioni, lakini huenda ikapungua au kuongezeka, itajulikana rasmi karibuni ni kiasi gani tutatumia, lakini awali ilikuwa Sh2 bilioni.”
Mohammed Dewji
Kuhusu uwekezaji wa mfanyabiashara maarufu, Mohamed Dewji (MO) ambaye amekuwa akitajwa kuitaka klabu hiyo , kiongozi huyo alisema suala lake halikuwa rasmi, bali mazungumzo ya pembeni.
“Mo hakuja rasmi kwetu, alikuwa akizungumza pembeni, hivyo, hatukuwa na sababu ya kusikiliza vitu ambavyo si rasmi, alibainisha kiongozi huyo.
Aveva alipoulizwa kuhusu MO, alisema aachwe apumzike kipindi hiki cha sikukuu.
Wakati huo huo, suala la kocha msaidizi wa timu yao, baada ya kuondoka kwa Seleman Matola, jukumu hilo limeachwa kwa kocha mkuu, Dylan Kerr.
Uongozi wa klabu hiyo umeeleza kutokuwa tayari kumwingilia kocha huyo na kusisitiza kuwa atakapokuwa tayari yeye ndiye ataupa uongozi taarifa za kocha aliyempata.
Ushindi wa juzi wa Simba dhidi ya Ndanda umempa Kerr aliyeuelezea kuwa umempa nguvu ya kutetea taji kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, ambako timu hiyo itakata utepe na Jamhuri ya Pemba kesho usiku.
Imani Makongoro/ Mwananchi
0 comments:
Post a Comment
Want to comment? write down here