Pages

Sunday, 24 January 2016

Marseille yajitosa kumtaka Samatta


Dar es Salaam. Wakati timu za Nantes na RCK Genk zikiendelea  kupigana vikumbo kwa ajili ya kuinasa saini ya mshambuliaji, Mbwana Samatta, klabu ya Olympique de Marseille nayo imejitosa kumuwania mshambuliaji huyo.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe la Ufaransa, Marseille imetajwa kuwa na tatizo kubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji na inaamini ikimpata Samatta aliyefunga mabao 19 katika mechi 35 msimu uliopita, atakuwa tiba ya tatizo lao.

Uamuzi wa Marseille kuingia kwenye mbio za kumuwania Samatta umekuja baada ya kubaini kuwa hakuna timu yoyote kati ya Nantes na Genk ambayo ina uhakika wa asilimia mia kumchukua mshambuliaji huyo., Hhivyo, wanaamini kuwa wanaweza kubadili mawazo ya Samatta na kumnasa kwenye kipindi hiki cha uhamisho wa dirisha dogo barani Ulaya.

“Marseille inaamini kuwa ina nafasi kubwa ya kumnasa mshambuliaji huyo na kumfanya awe staa, na inajivunia kutoa ofa kubwa ya fedha kuzidi ile iliyotolewa na Genk pamoja na Nantes. Inaonekana inaweza kuzipiku Genk na Nantes kwani wanaamini wana uwezo mkubwa wa kuishawishi Mazembe,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati huohuo, klabu ya Nantes nayo haijakata tamaa ya kumpata Samatta, ikidaiwa kupambana usiku na mchana kuhakikisha mchezaji huyo anamwaga wino na kujiunga nayo na kuipiga chini ofa iliyotolewa na klabu ya Genk.

Mtandao wa French 20minutes uliandika kwamba, kocha wa Nantes, Michel Der Zakarian amekuwa akivutiwa na kiwango cha Samatta na anaamini kuwa kumnasa mshambuliaji huyo kutaongeza nguvu kwenye kikosi chake.

Nantes imepania kushinda vita ya kumnasa Samatta na kuziacha kwenye mataa Genk na Marseille.

Charles Abel / Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here