Pages

Showing posts with label TFF. Show all posts
Showing posts with label TFF. Show all posts

Saturday, 16 April 2016

Waamuzi waibana TFF


KAMATI ya Waamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema kuwa haikubaliani na maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya kuwasimamisha waamuzi waliochezesha mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza kati ya JKT Kanembwa FC dhidi ya Geita Gold na Polisi Tabora dhidi ya JKT Oljoro.

Pia kamati hiyo ipo tayari kuwasaidia waamuzi hao waliosimamishwa wakituhumiwa kupanga matokeo iwapo watakuwa tayari kukata rufaa.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Salum Chama, alisema kuwa wakati suala hilo likifanyiwa uchunguzi na Kamati ya Nidhamu, hakuna mwamuzi yeyote mkongwe au aliyekuwepo katika kamati yao aliyeitwa ili kutafsiri mipaka na kanuni za kazi zao.

Alisema wao kamati ya waamuzi wamekuja kusikia maamuzi yakitolewa pasipo kushirikishwa jambo ambalo halipo kisheria lakini pia maamuzi yaliyotolewa hayakuwa na haki kwani hakuna ushahidi wa kutosha uliowakamatisha waamuzi hao.

“Kuanzia mwanzo hadi mwisho wa sakata lile hakuna aliyeshirikishwa katika kamati yetu, jambo ambalo kwa upande fulani si haki kwani na sisi tuna sheria na kanuni zetu ambazo tunazitumia uwanjani, lakini pia hadi hivi sasa hakuna ushahidi wa kutosha ni vipi wamekutwa na tuhuma za upangaji matokeo.

“Sisi kamati ya waamuzi, tupo tayari kuwasimamia bega kwa bega  iwapo kama wenyewe wanaona hawakutendewa haki na wakakata rufaa, lakini wakiomba tuwasimamie katika hilo tupo tayari,” alisema Chama.

Hivi karibuni Kamati ya Nidhamu ya TFF chini ya Makamu Mwenyekiti wake Wakili, Jerome Msemwa, iliwafungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh Mang’ola, kamisaa wa mchezo huo, Moshi Juma pamoja na mwamuzi wa mchezo kati ya Polisi Tabora dhidi ya JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na mwamuzi wa akiba, Fedian Machunde, waliofungiwa kwa muda wa miaka kumi  pamoja na kutozwa faini ya shilingi milioni kumi kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya upangaji matokeo kwenye michezo hiyo.

NA ZAINAB IDDY/ MTANZANIA

Wednesday, 6 April 2016

Takukuru yatua TFF

Ofisi za TFF jijini Dar es salaam.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), imesema inazo taarifa zote juu ya tuhuma za rushwa ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na tayari imeanza uchunguzi.

Kwa zaidi ya mwezi sasa kumekuwa na tuhuma za rushwa ndani ya shirikisho hilo baada ya kumalizika kwa mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza Kundi C zilizohusisha timu za Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Kanembwa na JKT Oljoro.

Suala hilo limeifanya Kamati ya Nidhamu ya TFF kuwafungia maisha na kuwasimamisha kwa miaka kumi baadhi ya viongozi wa soka na wachezaji.

Aidha baada ya adhabu hiyo, juzi kwenye mitandao ya kijamii zilisambaa sauti zinazodaiwa kuwa za baadhi ya viongozi wa TFF wakipanga matokeo ya moja ya mechi hizo.

Akizungumza na gazeti hili jana, msemaji wa Takukuru, Tunu Mleli, alisema taarifa wanazo na wanazifanyia kazi.

“Ndiyo taarifa tunazo na tumeshaanza uchunguzi.. ile ‘clip’ (ya sauti za wanaodaiwa viongozi wa TFF kupanga matokeo) imetufikia na tunaitumia kwenye uchunguzi wetu, lakini siwezi kusema utakamilika lini kwa sababu uchunguzi ni jambo endelevu na lipo kisheria zaidi, kwa hiyo tunachunguza ukishakamilika tutatoa taarifa,” alisema.

Kamati ya nidhamu ya TFF chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Jerome Msemwa iliwafungia kujihusisha na soka maisha viongozi saba wa mchezo huo kwa kuhusishwa na upangaji matokeo katika mechi za Kundi C.

Mbali na kufungiwa kwa viongozi hao kamati hiyo pia imefungia wachezaji wawili na waamuzi wawili kujihusisha na soka kwa miaka 10 kila mmoja huku wakipigwa faini ya Sh milioni 10 kila mmoja.

Aidha, kamati hiyo imezishusha mpaka daraja la pili timu za Geita Gold, iliyokuwa ipande Ligi Kuu, JKT Oljoro ya Arusha na Polisi Tabora, huku JKT Kanembwa ya Kigoma ikishushwa mpaka hatua ya ligi ya mkoa (RCL). Kanembwa ilishika nafasi ya mwisho katika kundi na tayari ilishashuka daraja.

Waliofungiwa maisha ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (Tarefa), Yusuph Kitumbo na Katibu wake, Fateh Rhemtullah, Mwenyekiti wa JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernard Fabian.

Wengine waliofungiwa maisha ni mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC na Geita Gold, Saleh Mang’ola, Kamisaa wa mchezo huo, Moshi Juma na kocha msaidizi wa Geita Gold, Choki Abeid.

Kwa upande wa wachezaji waliofungiwa miaka 10 ni kipa Mohammed Mohammed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Geita Gold huku wakitakiwa kulipwa faini ya Sh milioni 10 kila mmoja.