Pages

Wednesday, 6 April 2016

Takukuru yatua TFF

Ofisi za TFF jijini Dar es salaam.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), imesema inazo taarifa zote juu ya tuhuma za rushwa ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na tayari imeanza uchunguzi.

Kwa zaidi ya mwezi sasa kumekuwa na tuhuma za rushwa ndani ya shirikisho hilo baada ya kumalizika kwa mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza Kundi C zilizohusisha timu za Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Kanembwa na JKT Oljoro.

Suala hilo limeifanya Kamati ya Nidhamu ya TFF kuwafungia maisha na kuwasimamisha kwa miaka kumi baadhi ya viongozi wa soka na wachezaji.

Aidha baada ya adhabu hiyo, juzi kwenye mitandao ya kijamii zilisambaa sauti zinazodaiwa kuwa za baadhi ya viongozi wa TFF wakipanga matokeo ya moja ya mechi hizo.

Akizungumza na gazeti hili jana, msemaji wa Takukuru, Tunu Mleli, alisema taarifa wanazo na wanazifanyia kazi.

“Ndiyo taarifa tunazo na tumeshaanza uchunguzi.. ile ‘clip’ (ya sauti za wanaodaiwa viongozi wa TFF kupanga matokeo) imetufikia na tunaitumia kwenye uchunguzi wetu, lakini siwezi kusema utakamilika lini kwa sababu uchunguzi ni jambo endelevu na lipo kisheria zaidi, kwa hiyo tunachunguza ukishakamilika tutatoa taarifa,” alisema.

Kamati ya nidhamu ya TFF chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Jerome Msemwa iliwafungia kujihusisha na soka maisha viongozi saba wa mchezo huo kwa kuhusishwa na upangaji matokeo katika mechi za Kundi C.

Mbali na kufungiwa kwa viongozi hao kamati hiyo pia imefungia wachezaji wawili na waamuzi wawili kujihusisha na soka kwa miaka 10 kila mmoja huku wakipigwa faini ya Sh milioni 10 kila mmoja.

Aidha, kamati hiyo imezishusha mpaka daraja la pili timu za Geita Gold, iliyokuwa ipande Ligi Kuu, JKT Oljoro ya Arusha na Polisi Tabora, huku JKT Kanembwa ya Kigoma ikishushwa mpaka hatua ya ligi ya mkoa (RCL). Kanembwa ilishika nafasi ya mwisho katika kundi na tayari ilishashuka daraja.

Waliofungiwa maisha ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (Tarefa), Yusuph Kitumbo na Katibu wake, Fateh Rhemtullah, Mwenyekiti wa JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernard Fabian.

Wengine waliofungiwa maisha ni mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC na Geita Gold, Saleh Mang’ola, Kamisaa wa mchezo huo, Moshi Juma na kocha msaidizi wa Geita Gold, Choki Abeid.

Kwa upande wa wachezaji waliofungiwa miaka 10 ni kipa Mohammed Mohammed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Geita Gold huku wakitakiwa kulipwa faini ya Sh milioni 10 kila mmoja.

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here