Pages

Sunday, 27 March 2016

Ubora, udhaifu Yanga, Azam kimataifa


Dar es salaam. Wakati Yanga na Azam zikijiandaa kukabiliana na vigogo vya soka Afrika kutoka kaskazini mwa bara hilo mwezi ujao, timu hizo zitabebwa au hata kuangushwa na washambuliaji, safu zao za ulinzi zinazohitaji marekebisho makubwa.

Yanga itacheza na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika Aprili 9 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Azam itaikabili Esperance ya Tunisia, Aprili 10 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Msimu huu, timu hizo zimeonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji ambazo ni nadra kutoka uwanjani bila bao kwenye mchezo wowote, huku pia zikiwa na viungo mahiri wanaozibeba kwenye mashindano, lakini kama watakuwa kwenye ubora wao.

Yanga inabebwa na washambuliaji, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Simon Msuva na wengineo ambao wamefunga mabao 51 hadi sasa kwenye Ligi Kuu, wakati Azam inaongozwa nao, Kipre Tchetche, John Bocco, Farid Mussa walioiwezesha timu yao kufunga mabao 37.

Waonavyo wadau wa soka
Hata hivyo, baadhi ya wadau wa soka wamekiri kuwa timu hizo zinao uwezo wa kufanya vizuri, ila zinapaswa kurekebisha kasoro ndogo kwenye safu zao za ulinzi ambazo zikiachwa zitawagharimu katika michezo hiyo.

Kocha msaidizi wa JKT Ruvu, Mrage Kabange alisema Yanga na Azam zina soka la kiwango kikubwa, lakini wanapaswa kuongeza juhudi uwanjani katika michezo hiyo, huku wakiamini kila kitu kinawezekana.

Kabange aliyewahi kuichezea Simba na kuzinoa klabu kadhaa nchini alisema timu hizo hazipaswi kuwaogopa wapinzani wao kwani soka la sasa si kama lile zamani ambalo lilikuwa zaidi la mazoea.

Alizitaka klabu hizo kupambana ili kuhakikisha zinaibuka na ushindi katika michezo yao ya nyumbani, zikiamini kuwa ugenini lolote linaweza kutokea, ikiwamo fitina za Waarabu.

“Yanga na Azam zinao washambuliaji wazuri wanaoweza kufunga mabao muda wowote na ubora wa hizo timu unabebwa na aina ya washambuliaji wao, lakini zina matatizo kwenye upande wa mabeki.

“Ukiangalia Yanga, mabeki wake kwanza hawajiamini, wana tatizo la kujipanga, wana papara na wana tatizo kwenye ukabaji na hilo linaweza kuwaletea madhara kwani Waarabu hutakiwi kuwaachia wacheze.

“Pia, Azam nao wana matatizo kwenye upande wa mabeki, angalia hata mechi yao iliyopita dhidi ya Bidvest ya Afrika Kusini, mabeki walizembea, hivyo timu zote zinatakiwa kurekebisha hilo haraka,la sivyo itawagharimu,” alisema Kabange.

Mchezaji wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa masuala ya michezo, Ali Mayay alisema Yanga inapaswa kupunguza makosa katika safu yao ya ulinzi, huku akiwataka viungo kuongeza umakini.

“Yanga imekuwa na makosa makubwa katika ulinzi, mabeki wao wengi wamepunguza umakini, pia safu ya kiungo nayo inapoteza mipira, hivyo kama wasiporekebisha makosa hayo watapata matatizo mbele ya Waarabu,” alisema Mayay.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella au Golden Boy alisema Yanga na Azam, zote ni timu nzuri lakini zinatakiwa kuwa na nidhamu ya juu ya mchezo ziatakpopambana na Waarabu.

“Siwezi kusema sehemu gani zina upungufu kwani wachezaji wa timu hizo hawana nidhamu ya mchezo, angalia kama Yanga walipokuwa Rwanda walicheza vizuri walipokuja nyumbani mechi ya marudiano walicheza ovyo, sasa wakicheza hivyo mbele ya Waarabu itawagharimu.

“Uzoefu nilionao unapocheza na Waarabu unatakiwa kuwa na nidhamu, kwa sababu timu za huko zinakuadhibu kutokana na makosa unayofanya.

“Azam na Yanga zinatakiwa kuzidisha umakini uwanjani na kusaidiana kwani hata kama eneo fulani mfano ni zuri kama timu haina umakini litaonekana baya,” alisema Mogella.

Oliver Albert, Mwananchi

Related Posts:

  • Simba yatakata TAIFA huku Yanga ikifungwa MKWAKWANI Simba leo imezidi kuwapa raha mashabiki wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4 - 0 dhidi ya African Sports uwanja wa Taifa Dar es salaam, huku Yanga ikilala kwa mabao 2 - 0 mbele ya Coastal Union uwanja wa Mkwakwani … Read More
  • Yanga yatinga nusu fainali Mapinduzi Cup Mabingwa wa Tanzania Bara Timu ya Yanga, wamefanikiwa kutinga hatua ya Nusu fainali kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa mabao ambayo yamefungwa na wachezaji Aboubakar na Malimi Busungu na kuwa kinara wa kundi … Read More
  • Niyonzima rasmi Yanga Sakata la Niyonzima kufukuzwa Yanga limechukua mwezi mmoja kabla ya wiki iliyopita kumalizana na kiungo huyo kuomba radhi ili aweze kurejeshwa kikosini. Yanga ilitangaza kuvunja mkataba na Niyonzima kwa madai kwamba … Read More
  • Niyonzima aitishia nyau Yanga Dar es Salaam. Kiungo Haruna Niyonzima ameipa Yanga siku nne kubadili uamuzi wa kumfukuza na baada ya hapo ataanika ukweli wa mgogoro wake na klabu hiyo. Wakati Niyonzima akisema hayo, katibu mkuu wa Yanga, Dk Jonas … Read More
  • Mayanja asuka mkakati kuimaliza Yanga KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja, amesema anaandaa mbinu mpya ili aweze kuifunga Yanga katika mchezo wao wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. M… Read More

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here