Dar es Salaam. Kiungo Haruna Niyonzima ameipa Yanga siku nne kubadili uamuzi wa kumfukuza na baada ya hapo ataanika ukweli wa mgogoro wake na klabu hiyo.
Wakati Niyonzima akisema hayo, katibu mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alisema jana kuwa pamoja na klabu hiyo kutompa rasmi barua ya kukatisha mkataba, uamuzi huo haujabadilika.
“Ni kweli hajapewa barua, inaandaliwa, atapewa wakati wowote na hivyo suala la kusema yeye bado ni mchezaji wetu anaweza kusema, hazuiwi,” alisema Tiboroha.
Kiungo huyo wa Rwanda alisisitiza kujua kinachoendelea juu yake ndani ya klabu hiyo na kueleza kuweka wazi kila kitu ndani ya siku nne.
Alisema hatambui kuachwa kwake, huku akisisitiza kuwa yeye bado ni mchezaji halali kwani bado hajapewa barua rasmi ya kuvunjiwa mkataba wake.
“Najua kinachoendelea, nilichopanga kukifanya nakijua, ingawa sitapenda kukiweka wazi sasa, ndani ya siku nne hadi Jumanne nitaweka wazi kila kitu juu ya mgogoro huo na hatma yangu kisoka,” alisema.
Aliongeza kuwa hivi sasa kila mtu anasema analojua kuhusu mgogoro wake na Yanga, lakini yeye ndiye anayejua kila kitu na kubainisha muda mwafaka ukifika hatakuwa na sababu ya kuficha ukweli zaidi ya kuweka wazi nini kinachoendelea.
“Sijali kwa kinachotokea, haya ni mapito, lakini ukweli naujua, nilikuwa kimya nikijipanga, lakini ndani ya siku nne nitaeleza ukweli wangu na Yanga na nini nitafanya,” alisema.
Alieleza kuwa anatambua kila kitu kinachoendelea ndani ya klabu hiyo, lakini muda mwafaka ukifika ataweka wazi siri hiyo ya moyo wake.
Kuhusu kurejea APR ya Rwanda, kiungo huyo mchezeshaji alisema kila kitu ni utaratibu, ingawa hawezi kulizungumzia jambo hilo kwani bado anajua yeye ni mwajiriwa halali wa Yanga na bado anatambua mkataba wake na klabu hiyo.
Niyonzima alitupiwa virago Yanga kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukiuka makubaliano ya mkataba baada ya nyota huyo kuchelewa kujiunga na wenzake alipomaliza kuitumikia timu yake ya taifa ya Rwanda, Amavubi kwenye mashindano ya Chalenji nchini Ethiopia
Imani Makongoro / Mwananchi
0 comments:
Post a Comment
Want to comment? write down here