Pages

Thursday, 21 April 2016

Azam nguvu zote Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho


BAADA ya kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na Esperance ya Tunisia, kikosi cha Azam kimesema kwa sasa kinaelekeza nguvu zake kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na ile ya Kombe la Shirikisho (FA).

Mabingwa hao wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, walijikuta wakitolewa na Esperance katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya juzi usiku kukubali kichapo cha mabao 3-0.

Azam FC wakicheza bila ya Pascal Wawa, Kipre Tchetche na Jean Batista Mugiraneza, walijikuta wanaruhusu mabao hayo 3-0 katika kipindi cha pili na kutolewa kwa matokeo ya jumla ya bao 4-2 kwani mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, Wanalambalamba hao walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Himid Mao, amewaambia mashabiki wao kuwa kwa sasa nguvu zao zote wanahamishia katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) akiwaahidi kuwa watapambana kuchukua makombe yote hayo mawili.

“Matokeo yamewasikitisha watu wengi hata sisi wachezaji, lakini wanatakiwa wajue Azam FC ni timu changa sana na kwa sasa tunapiga hatua kubwa lakini hii haitufanyi tuvimbe vichwa kwani bado tuna deni, hivyo nafikiri inabidi tufanye kitu kikubwa zaidi kuweza kusogea mbele.

“Mashabiki waendelee kutupa sapoti kwani bado ligi ipo, FA pia ipo hivyo tutajitahidi kuweza kuchukua makombe yote hayo,” alisema.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuwasili nchini leo ambapo kitakwenda mkoani Shinyanga kucheza na Mwadui FC  mchezo wa nusu fainali michuano ya Kombe la Shirikisho (FA).

Azam FC iliyopanda Ligi Kuu miaka nane iliyopita, msimu huu ilikuwa ikishiriki kwa mara ya nne michuano ya Afrika hadi inafika raundi hiyo ilifanikiwa kuwatoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3.

Na Ezekiel Tendwa / Bingwa

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here