Pages

Sunday, 17 January 2016

Samatta kuvuta mawakala wengi Tanzania


BILA shaka kila mtu alisikia mshambuliaji wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani. Ushindi wake umeitoa Tanzania kimasomaso katika uso wa dunia, kwani ameitangaza vyema nchi yake.

Sio tu kuitangaza nchi yake, ametoa fursa kwa wachezaji vijana kujifunza kutoka kwake kwa kujituma na kupata mafanikio kama aliyoyapata yeye. Na moja ya mafanikio yake yametokana na nidhamu aliyoionesha tangu akiwa anasaka nafasi ya kucheza katika timu ya Simba na kuzidisha zaidi katika TP Mazembe. Anajivunia kuwa aliyewahi kuwa Kocha wa Simba Patrick Phir aliwahi kumtabiria mazuri kutokana na jinsi ambavyo alikuwa na moyo wa kipekee.

Ninaposema moyo wa kipekee inamaanisha alikuwa akitoka Mbagala kwa miguu na kukimbia hadi Karume kwenye mazoezi wakati huo akiwa amesajiliwa Simba. Kutokana na kuonesha nidhamu hiyo ya kuwahi mazoezini kila alipohitajika ni wazi kuwa hata Phiri aliona kuwa huyo ni kifaa. Sio tu kwa Simba bali anajivunia kuwa mmiliki wa timu ya TP Mazembe Moise Katumbi alikuwa akimpenda na kumuamini kutokana na nidhamu aliyoionesha katika kipindi chote alichotumikia timu hiyo.

Tofauti na wachezaji wengi ambao wamekuwa wakiendekeza starehe na pombe, kwa Samatta anasema yuko mbali na vitu hivyo. Ni mchezaji ambaye amebarikiwa na Mungu kwa kupenda kazi yake kuliko chochote na kudumisha nidhamu iliyomfanya kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani. Wapo wachezaji wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki wanacheza barani Ulaya na wana majina makubwa lakini hawakuwahi kupata tuzo hizo.

Ni bahati ya Samatta kuuonesha ulimwengu kuwa kuna nchi inaitwa Tanzania ina vipaji havifahamiki ili waitambue na kumiminika kwa wingi kutafuta vipaji vya soka. Watu wengi duniani wamekuwa wakiamini vipaji vya soka vipo katika nchi za Afrika Kaskazini na Magharibi na kumbe wakifanya uchunguzi na kufuatilia ukanda wa Afrika Mashariki wanaweza kuwapata wengi ambao hawajapata fursa hiyo.

Samatta amefanya vizuri lakini asiisahau timu yake ya TP Mazembe iliyomwonesha mwanga katika maisha yake kwani ndio iliyogundua kipaji chake mapema tu alivyojiunga na Simba na kupata bahati hiyo. Ni wazi kwamba kutokana na uwezo wa Samatta zipo timu nyingi za Afrika zitakuja kuangaza wachezaji wa kitanzania ikiwezekana kuwasajili katika klabu zao.

Mchezaji huyo amefungua njia kwa vijana wengine na sasa mawakala wengi kutoka kona mbalimbali watakuwa wanafuatilia soka la ukanda wa Afrika Mashariki kusaka vipaji. Mawakala ndio ambao wana mtandao na timu mbalimbali, watakuja kwa wingi kutafuta wachezaji Tanzania. Amefungua njia kwa wengine, kwa wale wenye malengo kama yake iwapo watazingatia nidhamu na kuonesha juhudi, hakika Mungu atawasaidia na kufika mbali kwani kinachohitajika na kujitoa kwa moyo bila kuchoka.

Wapo wengi hatuwajui na wengine wamekuwa wakikatishwa tamaa na watu wachache katika klabu zao, hawatakiwi kukata tamaa. Samatta anakwenda Ulaya katika nchi ya Ubelgiji kucheza katika timu ya Genk. Iwapo ataonyesha kiwango bora kama alichokionyesha TP Mazembe ataendelea kuitangaza nchi ya Tanzania kimataifa. Inawezekana siku moja kama Mungu atamjalia kucheza huko akaonekana katika timu nyingine kubwa za Ulaya na kusajiliwa.

Kama ilivyotokea kwa wachezaji bora wa Ulaya Lionel Messi na Christiano Ronaldo, hata kwa Samatta huenda siku moja Mungu akamjalia na kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa dunia iwapo ataendeleza juhudi zake. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema yanaweza yakawa ni maajabu ya dunia siku moja mchezaji huyo, akaingia katika kinyang’anyiro cha mchezaji bora wa dunia.

Yote yanawezekana kama mchezaji mwenyewe atakwenda kufanya kitu ambacho kimempeleka katika timu husika. Bado wenye uwezo kama Samatta wapo isipokuwa hawajapata fursa ya kucheza nje na wengine wakipata nafasi wanashindwa hata kwenda kwenye majaribio wakijazwa ujinga na timu zao kuwa watalipwa pesa nyingi ili wasiondoke na mwisho siku wanaelezwa viwango vyao vimeshuka.

Samatta amefungua njia kwa sababu mpango wake wa kutaka kwenda kucheza Ulaya, unatoa fursa kwa wengine wanaosaka nafasi ya kucheza katika bingwa huyo wa Congo kupata. Tayari baada ya yeye na Thomas Ulimwengu kuonesha kiwango, wachezaji kadhaa wamechukuliwa kwenda kufanya majaribio. Tumeona Haruna Chanongo na Abuu Ubwa wapo DRC wakisaka nafasi hiyo ya kucheza kabumbu TP Mazembe.

Iwapo watafanikiwa basi watacheza na kama wakijitahidi kama akina Samatta ni wazi kutaleta mafanikio makubwa katika nchi. Pia, wapo wachezaji kama Ibrahim Ajib wa Simba na Mohamed Ibrahim wa Mtibwa walioelezwa kutakiwa na timu hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa wale watakaoangukia kwenye bahati hiyo, wataendeleza yale mazuri yaliyofanywa na Samatta.

Kuna mchezaji kama Elias Maguli aliyekwenda kufanya majaribio Misri katika timu ya Al Ahly hivyo, jaribio lake likifuzu naye ataitangaza Tanzania huko. Maguli ana bahati na nchi za kiarabu kwani alipokuwa anacheza Ruvu Shooting aliwahi kwenda Qatar kwenye majaribio lakini hakufanikiwa. Huenda mpango wake kwa sasa ukafanikiwa baada ya kuonyesha kiwango bora alipokuwa katika timu ya Stand United na timu ya taifa ya Tanzania.

Wachezaji wote hao wanahitaji kuonesha uwezo kama wa Samatta ili kuendelea kuwaleta mawakala ambao wanakuja kwa wingi nchini kutafuta vipaji vitakavyocheza nje ya nchi. Mchezaji mwingine ni Farid Mussa wa Azam Fc naye pia anahitaji kupewa nafasi baada ya kuonesha kiwango bora msimu huu akiwa katika timu yake hiyo lakini pia, timu ya Taifa.

Hivi karibuni kulikuwa na tetesi kuwa atakwenda kufanya majaribio Slovenia lakini ghafla ikaelezwa kuwa atatafutiwa timu nyingine hivyo hataenda. Vijana hao wana ndoto kama za Samatta, wanahitaji kuruhusiwa na timu zao katika kuhakikisha wanafika mbali kisoka. Kuna Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liingilie kati na kutafuta mawakala kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji kufika mbali kwani peke yao hataweza. Kila la heri la Samatta!

Habari : Habari Leo
Picha kwa msaada wa Mtandao

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here