Mfungaji wa bao pekee la Yanga katika mchezo wa jana, Simon Msuva.
TIMU ya soka ya Yanga jana ilimaliza mechi zake za viporo vyema kwa ushindi na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wake wa mwisho wa viporo vyake vitatu ilivyokuwa navyo.
Jumatano Yanga iliifunga Mwadui ya Shinyanga mabao 2-1 katika uwanja huohuo na kabla ya hapo Yanga iliifunga pia Kagera Sugar mabao 3-1. Kutokana na matokeo ya jana, Yanga imefikisha pointi 59 na imechupa kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza ikiiengua Simba yenye pointi 57.
Timu zote zimecheza mechi 24. Hata hivyo Simba inaweza ikarejea kileleni tena leo kama itashinda mchezo wake wa raundi ya 25 dhidi ya Toto Africans utakaofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Bao pekee la Yanga katika mchezo huo lilifungwa dakika ya 47 na Simon Msuva kwa shuti la mbali kutokana na mpira wa adhabu ndogo aliopasiwa na Haruna Niyonzima. Adhabu hiyo ilitokana na beki Andrew Vicent kumchezea madhambi Deus Kaseke wa Yanga.
Yanga itajilaumu kwa ushindi mwembamba kutokana na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga, ambazo washambuliaji wake wakiongozwa na Donald Ngoma walishindwa kuzitumia.
Nayo Mtibwa ilipata nafasi za kufunga, lakini umaliziaji ulikuwa butu kwa kushindwa kulenga lango ama kupiga mipira dhaifu iliyodakwa na kipa Deogratias Munishi ‘Dida’. Kipigo hicho kimeifanya Mtibwa ibaki nafasi ya nne ikiwa na pointi 43 kwa michezo 26 iliyocheza.
Yanga sasa itaelekea nchini Misri kwa ajili ya kurudiana na Al Ahly Jumatano mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo mchezo wa kwanza uliofanyika Jumamosi wiki iliyopita Dar es Salaam timu hizo zilifungana bao 1-1. Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan/Malimi Busungu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke/ Amissi Tambwe.
Mtibwa Sugar: Said Mohamed, Ally Shomari, Majaliwa Shaaban, Andrew Vincent, Salim Mbonde/Boniface Maganga, Shaaban Nditi, Shiza Kichuya/ Vincent Barnabas, Muzamil Yassin, Ibrahim Rajab ‘Jeba’/Henry Joseph , Suleiman Rajab na Kelvin Friday.
NA MOHAMED AKIDA/ habari leo
0 comments:
Post a Comment
Want to comment? write down here