Pages

Wednesday, 23 December 2015

Mimi bado rais halali Fifa, adai Blatter


Zurich, Uswisi. Siku moja baada ya kufungiwa miaka minane, aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter ameibuka na kueleza kuwa yeye bado ni kiongozi wa shirikisho hilo.

Alieleza kuwa haoni kosa lolote kiasi cha kumtia hatiani na kufungiwa miaka minane.

Alitetea malipo kwa swahiba wake, Michel Platini ambaye kwa pamoja wamefungiwa miaka minane.

Bosi huyo mwenye umri wa miaka 79 raia wa Uswisi alieleza kuwa ataendelea kuwa rais wa Fifa, hadi suala lake litakapoamuliwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) mjini Nyon.

Juzi, kamati ya maadili ya Fifa chini ya Jaji Hans-Joachim Eckert, raia wa Ujerumani iliamua kuwa fungia licha ya kuwasilisha pingamizi dhidi ya uamuzi huo.

Blatter alitiwa hatiani kwa kumlipa Platini, rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Faranga za Uswisi 2 milioni (Pauni 1.35 milioni) mwaka 2011, ikiwa ni miaka tisa tangu wawili hao wadai kuwa na mkataba wa kazi ya ushauri ambayo ilistahili malipo hayo.

Mbali ya kufungiwa, Blatter alitozwa faini ya Faranga 50,000 au Pauni 34,000 na Platini, Faranga 80,000 au Pauni 54,000 kwa kosa hilo.

Akizungumza na wanahabari juzi mjini Zurich, Blatter akiwa na binti yake, Corinne alidai kuwa ameonewa.

“Kusema kwamba ni siku nzuri kwangu au Fifa, nitakuwa nimekosea,” alieleza Blatter.

“Huwezi kueleza kwamba mimi ni mtu anayetaka kujikosha. Mimi na mwanasheria wangu, tuliamini kuwa tumewaridhisha wanajopo, chini ya Jaji Eckert, tumewaeleza kila kitu kuhusu malipo. Tulifikiri kuwa kila kitu kilikuwa wazi.

“Tulikuwa na mkataba. Mkataba wa mwaka 1998 baada ya fainali za Kombe la Dunia. Kilichonishangaza ni uamuzi ambao umefikiwa dhidi yetu ambao haujazingatia makubaliano yaliyokuwapo. Mkataba huo ulithibitishwa na pande zinazohusika. Kulikuwa na ushahidi wa kufikiwa kwa makubaliano.

“Kwa hiyo, malipo hayo kwa Platini yalifanyika kulingana na kanuni za fedha kupitia kamati ya fedha, kamati tendaji kwa nia njema. Haikuwa hisani. Ni zawadi. Tuliepuka suala la rushwa. Tulifanya hivyo kulingana na kanuni za hesabu za Fifa.

“Unaweza kuwa na mkataba wa makubaliano ya mdomo. Safari ijayo, tutakwenda kwenye kamati ya rufaa. Ttutakwenda CAS,” alisema Blatter.

Kauli ya Platini
Naye Platini alidai kuwa atakwenda CAS ambako atakata rufaa kupinga uamuzi huo wa uonevu waliofanyiwa.

Alieleza kuwa dhamira yake ina amani. Alitaka hatua zichukuliwe kusafisha dhamira yake ambayo imechafuka.

Alieleza kuwa uamuzi huo unachafua sifa yake, unaua dhamira yake ya kugombea urais wa Fifa katika uchaguzi ujao.

Alisema kuwa alijua kuwa kamati hiyo isingeweza kuwatendea haki kwani kabla ya kumsikiliza Desemba 18 ilikuwa tayari imeamua adhabu.

Alisema uamuzi huo unalenga kumwondoa yeye katika ulimwengu wa soka. Blatter alitua mbele ya kamati ya maadili Alhamisi na kesho yake Platini alifika kwa ajili ya kujieleza ambako alieleza kuwa yeye alikuwa kama mpigania haki na marehemu Nelson Mandela aliyekuwa mtetezi wa haki, lakini hakupendwa na maadui zake kiasi cha kufungwa maisha jela.

Habari : Mwananchi
Picha: Kwa msaada wa Mtandao

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here