Pages

Saturday 16 April 2016

Simba kushiriki michuano ya kimataifa


TIMU ya Simba imethibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Nile Basin Championship, itakayoanza Mei 22 mwaka huu nchini Sudan.

Katika mashindano hayo mwaka huu, bingwa atajinyakulia zawadi ya dola za Kimarekani 30,000 sawa na Sh 65,697,000 huku mshindi wa pili akizawadiwa dola 20,000 (sawa na Sh 43,798,000 wakati mshindi wa tatu akipata dola za Kimarekani 10,000 (sawa na Sh 21,899,000).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mashindano hayo hushirikisha timu zilizomaliza ligi zikiwa nafasi ya tatu na kwa kuwa Simba katika msimu uliopita ilimaliza Ligi Kuu Tanzania Bara katika nafasi hiyo, hivyo wamepewa jukumu la kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo.

Mashindano ya Nile Basin yanashirikisha klabu kutoka katika nchi wanachama wa Cecafa ambazo ni Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania Bara na Zanzibar

Kwa mara ya kwanza Tanzania iliwakilishwa na Mbeya City katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mwaka 2014, ambapo wakiwa chini ya kocha wao, Juma Mwambusi, ilijikuta ikiishia hatua ya robo fainali.

Mbeya City ilifanikiwa kuingia katika hatua hiyo ya robo fainali kwa jumla ya pointi 4 nafasi ya pili lakini ikajikuta ikitolewa na Victoria University kwa bao 1-0 ambaye pia ndiye bingwa mtetezi wa michuano hiyo kwa mwaka 2014 baada ya kuwafunga AFC Leopards ya Kenya kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.

NA ZAINAB IDDY/HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here