Pages

Friday 26 February 2016

Yanga yatangaza raha


WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, leo wataikabili Cercle de Joachim ya Mauritius ukiwa ni mchezo wa marudiano hatua ya awali.

Katika mchezo wa kwanza ugenini Uwanja wa George V, Yanga ilishinda bao 1-0, matokeo ambayo yanawapa Yanga kazi nyepesi leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutinga hatua inayofuata kwani inahitaji angalau sare.

Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm, amejitapa kushinda mchezo huo baada ya maandalizi mazuri waliyofanya kwa wiki mbili tangu warejee nchini.

Pluijm ambaye katika mchezo huo atawakosa nyota watatu wakiwemo wawili wa kimataifa, Haruna Niyonzima na mfungaji wa bao pekee lililowapa ushindi ugenini Donald Ngoma, alisema pamoja na kuhitaji sare, lakini lazima washinde.

“Tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda mchezo wa kesho (leo), kwa sababu tumefanya maandalizi ya kutosha na tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki wetu hatutapenda kuwaangusha na kizuri zaidi tunawajua vizuri wapinzani wetu,”alisema Pluijm.

Pluijm alisema pamoja na kuwakosa nyota hao, lakini ana imani kubwa na wachezaji waliopo ambao ana hakika watacheza kwa kiwango cha juu na kuwapa ushindi. Wapinzania wa Yanga, Cercle de Joachim, tayari wametua Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo huo huku wakionekana wamejipanga kuhakikisha wanalipa kisasi.

Kocha wa timu hiyo, Abdel ben Kacem, amesema amewajua vizuri Yanga na kwa maandalizi waliyoyafanya anaamini atafanikiwa kulipa kisasi. Katika hatua nyingine, kocha wa Simba, Jackson Mayanja, ameitabiria ushindi Yanga katika pambano la leo kwani wapinzani wao ni timu ambayo haina jina kubwa katika soka.

“Sitaki kuizungumzia sana Yanga, lakini nawapa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, kwa sababu wana timu nzuri na tayari wana akiba ya bao kufuatia ushindi walioupata ugenini, lakini hata timu wanayocheza nayo ni dhaifu,” alisema Mayanja.

MOHAMED AKIDA/HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here