Pages

Saturday 30 January 2016

Man United waishinda Derby katika FA


Manchester United wamempunguzia shinikizo meneja wao Louis van Gaal kwa kulaza klabu ya Derby 3-1 katika raundi ya nne ya Kombe la FA.

Van Gaal alipuuzilia mbali habari kwamba alikuwa radhi kujiuzulu baada ya klabu yake kushindwa na Southampton Jumamosi, na timu yake ilicheza vyema dhidi ya klabu hiyo ya ligi ya Championship.

Wayne Rooney alifunga kwa kombora alilolitoa akiwa hatua 20 kutoka kwa goli na kuwaweka United mbele dakika ya 16 kabla ya George Thorne kupenya safu ya ulinzi ya vijana hao wa Van Gaal na kusawazisha dakika ya 37.

Kipindi cha pili Daley Blind aliwarejesha mbele baada ya kupokea krosi kutoka kwa Jesse Lingard dakika ya 65.

Juan Mata alikamilisha ushindi wao dakika ya 83.

Derby, ambao hawajashinda mechi yoyote katika ligi yao mwaka 2016 wanashikilia nafari ya tano katika ligi ya Championship, walitatiza United kidogo mwishoni mwa kipindi cha kwanza Thorne alipofikia mpira kutoka kwa Chris Martin.

Lakini kwa jumla, ulikuwa ushindi ambao ulitoa matumaini kwa timu hiyo ya Van Gaal, ambayo baada ya kutoshinda Desemba, imeshindwa mechi moja pekee Januari.

Isitoshe, ilikuwa mara ya kwanza kwa United kushinda mechi kwa kuwa magoli mawili mbele katika mechi 15.

Baada ya mechi, Van Gaal alisema: "Tulicheza vyema wakati uliofaa dhidi ya Derby. Tuliwazawadi goli lakini wakati wa mapumziko nilisema tulicheza vyema, niliwaambia wachezaji washikilie hapo na tungeshinda. Na tulishinda.”

Kwa upande wake, meneja wa Derby Paul Clement alisema: "Daima lazima uingiwe na wasiwasi kuhusu wachezaji nyota kama vile Juan Mata na Anthony Martial. Walikuwa hatari sana.”

Derby watakuwa wenyeji wa Preston Jumanne wakijaribu kufufua kampeni yao ligini, nao Manchester United watawakaribisha Stoke nyumbani Old Trafford jioni hiyo.

BBC Swahili

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here