Pages

Sunday 27 December 2015

Tambwe hazuiliki, Simba yajikwaa


Dar/Mikoani . Ni nani wa kumzuia Amissi Tambwe? Hilo ni swali linaloweza kuulizwa sasa na mashabiki, hali kadhalika mabeki wa timu pinzani baada ya jana mshambuliaji huyo wa Yanga kuifungia timu yake mabao mawili wakati timu yake ikiiadhibu Mbeya City kwa mabao 3-0, huku mtani wao, Simba ikikwama tena Kanda ya Ziwa.

Tambwe alimtungua mabao hayo kipa wa zamani wa timu hiyo na Simba, Juma Kaseja, dakika za 36 na 64, akitumia vyema pasi za Simon Msuva na beki Mwinyi Haji.

Kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko alikamilisha furaha kwa mashabiki wa Yanga kwa bao la tatu, dakika ya 66 na kufikisha mabao manne msimu huu.

Kwa idadi hiyo, Tambwe amefikisha mabao kumi akimpindua Elius Maguli wa Stand United ya Shinyanga aliyekuwa akiongoza aliyebaki na mabao tisa.

Shinyanga
Simba ambayo wiki iliyopita ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Toto Africans ya Mwanza katika mchezo ambao kocha Dylan Kerr alisingizia ubovu wa Uwanja wa CCM Kirumba uliojaa maji na utelezi kutokana na mvua iliyonyesha muda mfupi kabla ya mchezo huo, jana ililazimika kuchomoa bao dhidi ya Mwadui ya Shinyanga na kuambulia sare na pointi moja.

Kabla ya mchezo huo ambao kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwello ‘Julio’ aliapa kumfukuza kazi kocha wa Simba, Dylan Kerr kwa kipigo, alikaribia kucheka baada ya kiungo Nizar Khalfan kutangulia kufunga bao dakika ya 77. akimalizia kazi nzuri ya kiungo wa zamani wa Azam, Malika Ndeule.

‘Mtoto’ wa Azam, Brian Majwega akicheza mchezo wake wa kwanza akiwa katika uzi mwekundu aliisawazishia timu yake bao, dakika ya 85, akitumia mpira wa kiungo Mwinyi Kazimoto.

Tanga
Stand United ya Shinyanga iligeuka mwenyeji baada ya kuizima Coastal Union kwa mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Stand, ambayo moja iliyopita ililambishwa mabao 4-0 na Yanga, ilianza kusaka ushindi kwa bao la Haruna Chanongo, dakika ya 12, akitumia vyema pasi ya Hassan Banda, aliyeipa timu yake bao la pili, dakika ya 44.

Naye Frank Hamis aliiandikia Stand bao la tatu, dakika ya 55, lakini Coastal ilifuta machozi kwa bao la penalti, dakika ya 76 la Mnigeria, Abasilim Chidiebere, likiwa bao lake la kwanza msimu huu.

Msemaji wa Coastal, Oscar Assenga alisema timu yake ilizidiwa na wapinzani wao tangu dakika ya mwanzo na kupoteza mwelekeo, lakini ana imani makocha watarekebisha makosa hayo katika mechi zijazo.

Manungu
Vijana wa kocha Mecky Mazime, waliendelea kutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kuiadhibu Mgambo JKT ya Tanga kwa mabao 3-0. Mashujaa wao walikuwa kiungo Henry Joseph, dakika ya 16, Said Bahanuzi, dakika ya 48 na Shiza Kichuya, dakika ya 77 ya mchezo huo.

Mtwara
Wenyeji Ndanda waliambulia kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa vijana wa kocha Abdallah Kibaden, JKT Ruvu waliopachika mabao yao kupitia kwa Hamis Thabit, dakika za 24, 37 na Saad Kipanga, dakika ya 63 huku Atupele Green akifunga la kujiliwaza, dakika ya 46 ya mchezo huo.

Imeandikwa na Charles Abel (Dar), Masoud Masasi (Shinyanga), Salim Mohammed (Tanga), Haika Kimaro (Mtwara)
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Want to comment? write down here